Tuesday, May 24, 2016

AMANI NA UPENDO

Kiongozi mkuu wa kanisa
katoliki duniani Papa Francis
amekutana na kufanya
mazungumzo na Imam mkuu
wa msikiti wa Al-Azahr wa
nchini Misri ikiwa ni ishara
nzuri ya mahusiano baina ya
dini mbili. Mkutano huu
unatajwa kuwa wa kwanza na
wa kihistoria baina ya kiongozi
huyo wa kanisa katoliki na
kiongozi wa juu wa kiislamu.
Mahusiano baina ya kituo
hicho cha Al-Azhar kinachotoa
mafunzo ya kiislamu nchini
Misri na Vatican yalikatika
mwaka 2011 wakati ambapo
kiongozi wa kanisa katoliki wa
wakati huo Benedict wa 16
alipotajwa kurudia kuikashifu
dini ya kiislamu.
Uamuzi huo ulikuja baada ya
kauli ya Papa Benedict ya
kusema kulikuwa na "mkakati
wa vurugu uliowalenga
wakristo" baada ya watu 23
kuuawa katika shambulizi la
bomu lililotekelzwa nje ya
kanisa mjini Alexandria nchini
Misri.
Tangu kuchaguliwa kwake
mwaka 2013, Papa Francis
ameweka mkazo katika
kuboresha mahusiano baina ya
imani zote . Ameonekana
mwenye furaha wakati
alipomsalimia kiongozi huyo
Ahmed al-Tayeb.
Abbas Shuman , naibu imam
mkuu ameliambia shirika la
habari la AFP jana kwamba
ishara anazotoa Papa Francis
kwa Waislamu zimemshawishi
Tayeb kukutana nae.
Papa Francis amewaambia
waandishi wa habari kuwa
"mkutano wetu ni ujumbe ".
Papa Francis akifanya
mazungumzo na Imam Ahmed Al-
Tayeb mjni Vatican
Katika tamko juu ya ziara ya
Imam huyo, wanasema Sheikh
Tayeb amekubali kukutana na
Papa Francis katika jitihada
zake za kuendeleza amani.
Katika kauli iliyotolewa na
Vatican, inasema viongozi hao
pia wamejadili juu ya matatizo
ya ugaidi na machafuko
pamoja na hali ya wakristo
walioko mashariki ya kati na
namna nzuri ya kuwalinda.
Kuonyesha mfano kwa mataifa
ya magharibi , Papa Francis
amewapokea baadhi ya
wakimbizi waliokimbia vita
nchini Syria. Wiki iliyopita pia
aliyashuku mataifa ya
magharibi kwa kutaka kuiuza
aina yao ya demokrasia katika
mataifa ya Afrika na Mashariki
ya kati pasipo kuzingatia siasa
za ndani.
Mwaka jana Papa Francis
alitoa rai ya kukomeshwa kile
alichokiita kuwa mauaji ya
kimbari ya wakristo katika
eneo la mashariki ya kati
ingawa alionya kwamba
haikuwa sahihi kuwahusisha
waislamu na machafuko.
Wakristo wa madhehebu ya
koptiki ni asilimia 10 ya wakazi
wote wa Misri ambapo idadi
kubwa ni waislamu wa
madhebu ya sunni.

Share: